Zanzibar, Tanzania 0652510306 / 0796324831 info@jzqt.or.tz

Kumbukumbu Ya Sheikh

Historia Ya Sheikh

Muhammad Bin Nassor (R.A)

Sheikh Muhammad Nassor Abdulla Elqadiriy (R.A) alizaliwa mwaka 1925 katika kijiji cha Kibanguni, Makunduchi, Mkoa wa Kusini, Unguja. Baba yake alikuwa Sheikh Nassor bin Abdalla (R.A), aliyefariki dunia kabla ya Sheikh Muhammad kuzaliwa — hivyo akazaliwa akiwa yatima.

Mwaka 1939 alianza elimu ya msingi katika Shule ya Makunduchi, na mwaka 1946 aliendelea katika Skuli ya Sekondari ya Zanzibar Mjini. Hata hivyo, kutokana na maradhi ya macho, hakuweza kuendelea na masomo hayo, na mwezi Mei 1946 alijiunga na Chuo cha Ualimu cha Dole. Mwaka 1948 alianza kazi Serikalini, akihudumu katika nyadhifa mbalimbali kama Mwalimu, Mudiri (Mkuu wa Wilaya), na Balozi wa Tanzania nchini Marekani, Sweden, na Misri.

Wakati akiwa Marekani, alianza kuandika vitabu viwili vya Kiarabu — Tatwhiru Nufusi na Hidayatu Saliki (Ahlul Badr). Akiwa Misri, alipata fursa ya kufanya Hijja yake ya kwanza na kumzuru Sayyid Abdul Qadir Jailaniy (Q.S.A) huko Baghdad, Iraq. Mwaka 1949 alikutana na Sheikh wake wa roho, Sheikh Abdalla bin Ahmad (R.A), ambaye alimlea kiroho na kumjenga katika elimu ya ndani ya Tasawwuf na tiba za kiislamu.

Mwaka 1973 alisafiri hadi Somalia akiwa na Bwana Rashid Kibwana, ambako alikabidhiwa amana ya Joho (Juba), Kofia na Kashida Nyekundu — alama za Umakamu (Swahibu Sajjaada) — urithi kutoka kwa Sheikh Uwesu bin Ahmad (R.A), ambazo asili yake ni kwa Sayyid Abdul Qadir Jaylaniy (Q.S.A).

Sheikh Muhammad bin Nassor (R.A) alikuwa Kiongozi Mkuu wa Tariqatul Qadiriyya na mlezi wa roho za Waislamu (Muridi) wa Twariqa hiyo. Alirithi kazi hii takatifu kutoka kwa Sheikh Abdalla bin Ahmad (R.A), ambaye naye aliipokea kutoka kwa Sayyid Omar bin Qulatayni (R.A), hadi kufikia kwa Sayyid Abdul Qadir Jaylaniy (Q.S.A).

Alikuwa miongoni mwa Masheikh wakubwa duniani waliobobea katika elimu mbalimbali za Kiislamu — ikiwemo Qur'an, Tasawwuf, Fiqhi, Sira, Tajwid, Nahw, Sarf, Balagha, Lugha ya Kiarabu, Tafsiri ya Qur’an, na Hadithi. Kupitia elimu na malezi yake, alileta mwamko mkubwa wa kiroho na kielimu miongoni mwa Waislamu wa Afrika Mashariki na kwingineko.

Katika maisha yake, Sheikh Muhammad Nassor (R.A) aliwalea Muridi wake kwa upendo, uvumilivu, na hekima ya hali ya juu, akiwafunza njia nyepesi ya kufikia maarifa ya Mwenyezi Mungu. Alijenga misikiti, madrasa za Qur’an kwa watoto, watu wazima, na kina mama, na kuweka misingi ya kuanzishwa kwa vyuo vikubwa vya Kiislamu Bara na Visiwani.

Sheikh Muhammad Nassor (R.A) alifariki dunia mwaka 2003 na amezikwa katika Msikiti wa Ngamia, Mburahati kwa Jongo, jijini Dar es Salaam. Kazi zake, malezi yake, na misingi aliyotuachia vinaendelea kuwa dira ya Muridi na Waislamu wote wanaotafuta nuru ya kiroho. Tunamuomba Mwenyezi Mungu atujaalie kushikamana na mwenendo wake mwema na mafundisho yake matukufu. Amin.

  • Hadhara za Wakati wake
  • Ujenzi
  • Islamic Center
Sheikh Muhammad Nassor

Wasiliana Nasi

Zanzibar, Tanzania

info.jzqt.or.tz

0652510306 / 0796324831

Mengineyo

© www.jzqt.or.tz
Template Design: HTML Codex